Stori:  Mwandishi Wetu
 Bifu zito lipo hivi sasa kati ya Naibu Waziri wa Habari, Vijana, 
Utamaduni na Michezo, Amos Makalla na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven
 Ngonyani.
Gari la Amos Makalla aina ya BMW X5 ambalo linadaiwa kuchukuliwa na Profesa Maji Marefu.
Makalla anamtuhumu Ngonyani a.k.a Profesa Maji Marefu kuwa alichukua 
gari lake aina ya BMW X5 kisha akatokomea nalo kisha akawa anampigia 
simu hapokei na hata akimtumia SMS hajibu.
Kutokana na malalamiko hayo, hivi sasa Maji Marefu anasakwa na polisi
 wa Kituo cha Kati (Central), Dar es Salaam, tuhuma zikiwa ni wizi wa 
kuaminiwa, shauri lipo kwenye kitabu cha ripoti za polisi (Report Book 
‘RB’) kwa namba CD/RB/13336/2013.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.
NYEUPE NA NYEUSI YA TUHUMA ZENYEWE
 Nyeupe na nyeusi (black and 
white) ya tuhuma hizo, inawekwa wazi na ‘sosi’ wetu ambaye aliliibia 
siri gazeti hili kwamba sakata kati ya Maji Marefu na Makalla lilianza 
tangu Julai, mwaka huu wakati waheshimiwa hao walipokuwa ndani ya Jiji 
la Dar es Salaam.
“Maji Marefu aliomba gari la Makalla ili alitumie kwa mizunguko ya 
siku moja tu lakini hakurudisha,” kilisema chanzo chetu. “Mgogoro mkubwa
 ulianza kuibuka kuanzia hapo na mpaka leo waheshimiwa hao hawazungumzi 
kwa salamu wala kutakiana heri.”
Chanzo chetu kiliendelea kusema: “Siku ya kwanza tu ilipopita, 
Makalla alimpigia simu Maji Marefu akawa hapokei, akimtumia SMS hajibu. 
Kwa kifupi Makalla alipoteza mawasiliano na Maji Marefu lakini 
aliendelea kusubiri kwa sababu anajua ni mtu wake.”
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani.
Habari zaidi zinasema kuwa kilipita kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja 
bila ya Makalla kumpata Maji Marefu kwenye simu lakini walikutana katika
 Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioketi kati
 ya Agosti 27 hadi Septemba 13, mwaka huu, Dodoma.
“Walipokutana Makalla alimuuliza Maji Marefu gari lake lipo wapi? 
Maji Marefu alimjibu alilikabidhi Lamada Hotel, Dar es Salaam,” alisema 
mtoa habari wetu na kuongeza: “Unajua makabidhiano ya lile gari 
yalifanyika Lamada Hotel, kwamba angelirudisha baadaye lakini ikawa 
kimya.
“Hata hivyo, Makalla aliona siyo kesi kubwa, akafuatilia Lamada 
Hotel, menejimenti ya hoteli hiyo ilijibu kuwa gari hilo halijapelekwa 
pale. Vilevile baada ya kuzungumza siku hiyo, Maji Marefu alitoweka na 
bungeni hakuonekana tena.
“Baada ya kupata majibu hayo kutoka kwa Profesa Maji Marefu na 
Lamada, Makalla alifungua mashitaka Central, akidai kuibiwa gari lake na
 Maji Marefu.”
MAKALLA AFUNGUKA
 Makalla ambaye ni Mbunge wa Mvomero (CCM) 
alipozungumza na mwandishi wetu alikubali kila kitu kisha akafunguka: 
“Niliomba polisi wanisaidie maana kwa hali iliyokuwepo ni kama nilikuwa 
nimeshatapeliwa. Vilevile niliripoti kwa Kamanda Mohamed Mpinga (mkuu wa
 kikosi cha usalama  barabarani) ili naye awaambie vijana wake 
wanisaidie kunitafutia gari langu.
“Nilimpa alama zote, rangi na namba za usajili. Oktoba Mosi, mwaka 
huu, ikiwa ni karibu miezi mitatu imepita tangu nimpe gari, polisi Tanga
 waliliona gari langu likiwa linaendeshwa na mheshimiwa Ngonyani (Maji 
Marefu) kwenye msafara wa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
“Nilimtumia SMS kumwambia kuwa gari langu ameonekana nalo katika 
msafara wa makamu wa rais. Polisi Tanga walitaka kumkamata lakini 
nikaomba aachwe kwanza, kukamatwa katika msafara wa makamu wa rais 
angeona amedhalilishwa.
“Nilimuomba baada ya msafara akalikabidhi gari kwa RPC Tanga kwa 
sababu linatafutwa na polisi. Akaniambia hawezi kulipeleka polisi kwa 
sababu tulikabidhiana vizuri. Nikamwambia sitaki kwa sababu alikuwa 
ananizungusha sana kunirudishia gari langu, mara aseme amelipeleka 
Lamada kumbe bado analo na wakati huohuo hapokei simu wala hajibu SMS 
zangu.”
USHAHIDI WA SMS
 MAKALLA: “Mhe. pamoja na kutopokea simu na 
kutojibu meseji zangu, nakujulisha leo Oktoba Mosi, umeonekana na gari 
langu kwenye msafara wa makamu wa rais. Polisi walitaka wakukamate 
nikashauri wasubiri umalize mkutano. Kwa meseji hii naomba kesho asubuhi
 ukakabidhi gari langu kwa RPC Tanga, bila kukosa. Utamkuta ndugu Rajabu
 alipokee gari hilo baada ya ukaguzi mbele ya RPC.”
MAJI MAREFU: “Sawa nimekuelewa, yote ni makosa yangu na hii ni mali 
yako ila gari hatukupeana polisi, ungeniambia ulipo nikuletee.”
MAKALLA: “Sitaki umenizungusha sana, nilikukabidhi kwa heshima lakini umegeuka adui, hupokei simu huu ni mwezi wa tatu.”
MAJI MAREFU: “Ok nitafanya hivyo.”
MAKALLA ANAENDELEA
“Hakupeleka gari kwa RPC Tanga kama nilivyomtaka. Zilipita kama siku 
tatu, ndipo mtu mmoja akaenda kulitelekeza gari langu Lamada Hotel 
usiku. Walinzi walimuuliza yule mtu aliyetekeleza lile gari kwa nini 
anaacha gari na anakimbia? Hakujibu, akarukia kwenye pikipiki ambayo 
ilikuwa inalifuata lile gari kwa nyuma kisha akatoweka.
“Uongozi wa Lamada baada ya kuliona gari langu walinipigia simu, 
wakanijulisha nami nikapiga simu polisi, wakaenda kulichukua. Mpaka sasa
 gari lipo polisi central, wanasubiri kumkamata Mhe. Ngonyani ili kesi 
iendelee mbele.”
KAZI YA UWAZI
 Gazeti hili baada ya kuzungumza na Makalla, 
lilikwenda kufanya upekuzi wake central na kubaini kwamba kesi hiyi ipo 
na madai yapo kama yalivyoelezwa.
Baada ya hapo, mwandishi wetu alimpigia simu Maji Marefu ambaye 
alipokea akiwa Nairobi, Kenya, na aliposomewa tuhuma dhidi yake, 
alijibu: “Subiri nirudi Dar, nitaeleza kila kitu.” Mahojiano yalikuwa 
kama ifuatavyo;
MWANDISHI: Kuna madai kwamba ulichukua gari la Mheshimiwa Makalla, 
umekaa nalo miezi mitatu, kipindi chote hicho simu ulikuwa hupokei wala 
hujibu SMS zake.
 MAJI MAREFU: Siyo kweli.
 MWANDISHI: Labda ukweli ni upi.
 MAJI MAREFU: Labda kwa sababu sipo Dar, nisubiri nirudi tutakaa tuzungumze.
 MWANDISHI: Ungeniambia kwa kifupi tu ni kwa nini Makalla akushitaki, 
maana hii kesi ipo polisi, RB ipo na unatafutwa kwa tuhuma za wizi wa 
kuaminiwa.
 MAJI MAREFU: Polisi wananitafuta mimi?
 MWANDISHI: Ndiyo wanakutafuta wewe.
 MAJI MAREFU: Kwa vile nipo Nairobi na wewe upo Dar, naomba usubiri 
tukutane kwanza ndipo nitaweza kueleza ukweli halafu ndipo mtaamua 
kuendelea mbele.
 MWANDISHI: Sawa mheshimiwa, swali lingine wewe una ugomvi na Mheshimiwa Makalla?
 MAJI MAREFU: Aah, ndiyo nikasema tukikutana ndiyo italeta picha nzuri. Kama natafutwa au kuna tukio lolote nitaeleza.
 MWANDISHI: Sawa mheshimiwa, basi nijibu swali hili, wewe una ugomvi na Makalla?
 MAJI MAREFU: Sina ugomvi naye.
 MWANDISHI: Sasa kwa nini akushtaki kwa wizi wa gari lake?
 MAREFU: Naomba tukutane nikirudi nitaongea tu.
 MWANDISHI: Inasemekana hilo gari uliwahi kumwambia Makalla kwamba 
uliliacha Lamada Hotel lakini baadaye ukaonekana nalo kwenye msafara wa 
makamu wa rais Tanga. Hili limekaaje?
 MAJI MAREFU: Mimi nina magari 
zaidi ya 15, nitakupeleka uone kama mimi nina shida ya gari. Nyumbani 
kwangu kuna magari ya kila aina.
 MWANDISHI: Ni kweli Makalla alikukabidhi gari?
 MAJI MAREFU: Subiri nirudi Dar nitaongelea hilo.
 MWANDISHI: Nijibu tu hilo moja tu, alikupa au hakukupa?
 MAJI MAREFU: Kwani yeye anasema nilimnyang’anya au alinipa?
 MWANDISHI: Anasema alikupa.
 MAJI MAREFU: Sasa subiri nirudi nitaeleza ukweli wangu.
 MWANDISHI: Kwani mheshimiwa inashindikana nini kunijibu swali hili moja tu? Alikupa au hakukupa?
 MAJI MAREFU: Ukweli mtaupata nikisharudi Dar.
POLISI NAKO
 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, 
Kamishna Suleiman Kova, alipoulizwa kuhusu kesi hiyo, kwanza alisema 
hajapata taarifa yoyote kuhusu sakata hilo mpaka afuatilie.
Siku iliyofuata, Kova alipigiwa tena simu akaulizwa kuhusu sakata 
hilo, akajibu: “Kuna mtu wa Uwazi alinipigia simu jana kuhusu hii kesi, 
unajua mimi ni kamishna, hii kesi ni ndogo na siyo kila kesi lazima 
nijibu mimi.