Social Icons

Thursday, May 10, 2012

FAIDA YA KUFANYA KAZI AU SHUGULI INAYODHARAULIWA.....


BINADAMU wengi wana tabia ya kuchagua vitu na hasa vizuri kwa lengo la kulinda heshima yao mbele ya wenzao. Kwa tabia hiyo ya utukufu wengi wetu tunapenda kuwa na kazi nzuri si itakayotusaidia kuishi bali kukidhi heshima yetu mbele ya jamii.
Vijana wengi waishio hasa maeneo ya mijini wako radhi kuishi maisha ya kubangaiza kwa kukaa vijiweni kupiga soga na kuvuta bangi lakini si kwenda kuuza mboga za mitaani, kubeba zege kwenye kandarasi za ujenzi au kuuza maji kwenye mikokoteni.

Hawataki kazi au shughuli zinazochukuliwa kama fedheha licha ya kwamba wanaozifanya wanajipatia kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao kwa sababu tu ya ule umwinyi mkuu wa kutaka utajo mzuri mbele za watu.
Nayasema haya kwa sababu miaka michache tu iliyop ita mimi pia niliishi kwenye utumwa huu wa utukufu, nilijiona siwezi kufanya kazi dhaifu hata kama zina kipato, kwa fikra tu kwamba akiniona msichana fulani pale mtaani atanidharau. Kumbe kwa upande mwingine nilidharaulika zaidi kuliko hata nilivyojikinga kwa kukwepa kazi.

Kwa namna yoyote ile, heshima ya mtu ni kazi na mafanikio ndiyo kipimo cha akili. Hii haijalishi unafanya shughuli ya heshima kimtazamo au yenye kudharauliwa na wengi kimawazo.
Haiwezi kutokea kijana muuza maji aliyejenga nyumba yake ya vyumba vitatu na kujiendeshea maisha yake akadharauliwa na mfanyakazi wa benki anayetangatanga kwa ufujaji wa fedha na kukosa tija ya maisha, akaheshimiwa kwa lemba la kazi yake tu. Kamwe hilo haliwezekani.

Ikiwa ni hivyo, kwa nini watu wanachagua kazi? Je, hatuna ushuhuda wa mafundi viatu kuwa na nyumba, miradi na biashara kubwa huku wafanyakazi maofisini wakigeuka wakopaji kwenye maduka ya Wamachinga wanaotembeza nguo mikononi kwenye mitaa ya mijini? Naamini ushahidi upo wa kutosha.

Maeneo mengi ya wakulima wa zao la tumbaku katika mkoa wa Tabora, kwa mfano, na vijana wanaomiliki maduka madogomadogo maarufu kama vioski ni wageni ambao walifika kwenye mkoa huo kama watumishi au wasaidizi wa mashambani, wakifanya kazi dhaifu ambazo wenyewe huzitafsiri kama shughuli zisizokuwa na heshima. Lakini pato la kazi hizohizo ndilo hatimaye huwapatia vioski ambavyo wenyeji huenda kukopa bidhaa.

Katika hali ya kawaida, kazi zinazoonekana dhaifu ni funzo kubwa sana katika maisha na mara nyingi hujenga ari ya aina yake katika uwajibikaji wenye lengo la kujikomboa na hiyo zana ya kudharaulika.
Watu wengi matajiri historia zao huanzia kwenye kazi dhaifu. Huko ndiko kulikowafunza nidhamu ya matumizi ya fedha. Kwenye dharau kumejaa maarifa na mbinu za ukombozi kuliko mahali penye maisha ya heshima ambako hupumbaza na kuwafanya wahusika wasipige mbio kuelekea kwenye mafanikio zaidi.

Wito wangu kwa vijana wenzangu, Watanzania wote, tusikubali kuishi na ufalme, heshima na utukufu usioweza kutusaidia, badala yake tukubali kufanya kazi hata zinazoonekana dhaifu kwa lengo la kujipatia kipato ili hatimaye tutafsri hali ya kudharauliwa kuwa heshima.


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment

 

for more information call us

+255718953088
-------or-------
+255784953088
*email*
innocentfabian@gmail.com
THANKS

quote of the day

"Don't criticize me simply because I am different. Understand me, and you will most likely appreciate my difference and criticize your variance."