Mapenzi ni mhimili muhimu sana katika maisha ya binadamu. Mtu asiyeyapa maanani, huyo ana kasoro zake na kamwe hawezi kuyafurahia maisha.
Mapenzi hasa unapofanikiwa kumpata mtu sahihi, yana raha yake. Unaweza kujikuta unanenepa tu kutokana na kuwa na mtu anayeonesha mapenzi ya kweli kwako, kukujali na kukuthamini katika shida na raha.
Hata hivyo, mapenzi ya sasa yamebadilika sana, yamekuwa ni tofauti na yale yaliyokuwepo enzi za mababu zetu. Siku hizi hakuna mapenzi, usanii na ulaghai vimetawala kiasi kwamba akitokea mtu akakuambia anakupenda huwezi kumuamini mara moja.
Kwa nini mada hii?
Rafiki yangu ambaye siwezi kumuanika hapa kwa sasa yupo kwenye penzi la kuibiwa. Mpenzi wake ambaye walikuwa na malengo ya kuoana kamfanyia kitu ambacho kimeniuma licha ya kwamba siye niliyetendwa. Nilikuwa nikiwaona jinsi wanavyopendana kwa dhati, hakukuwa na mazingira ya unafiki kabisa.
Kila mmoja alijitahidi kuonesha upendo wake kwa mwenzie kiasi kwamba penzi lao mara kwa mara nilikuwa nikilichukulia kama mfano wa kuigwa. Hizi I love you, I miss you zilikuwa hazikauki kwao. Yote tisa, wapenzi hawa walikuwa wakiaminiana sana, yaani kila mmoja aliamini mwenzake hawezi kumsaliti.
Kilichotokea juzi ndicho kilichonisukuma kuandika makala haya na hapo ndipo utajua mapenzi ya sasa asilimia kubwa ni ya Kichina. Wakati rafiki yangu kasafiri, mimi kwa macho yangu nilimshuhudia yule dada akiingia gesti na mwanaume mwingine. Niliumia sana kana kwamba mimi ndiye niliyekuwa nimesalitiwa.
Hata hivyo, sikutaka kuwa chanzo cha wawili hao kuachana, nikabaki na siri yangu moyoni mpaka leo. Kinachoniumiza zaidi ni kwamba, yule jamaa karudi na mapenzi yao yako vile vile. Jamaa anajisifia kuwa anapendwa lakini kumbe mapenzi ni ya Kichina.
Tunajifunza nini?
Usanii katika mapenzi sasa unachukua nafasi kubwa sana. Dada zetu wengi wao wako kifedha zaidi. Unamkuta anajifanya kukupenda sana kumbe hakuna chochote, wizi mtupu!
Wanaume nao usiseme, si ajabu ukamkuta akionesha mapenzi ya ajabu kwa msichana na kufikia hatua ya kuahidi ndoa lakini kumbe lengo lake ni kuonja penzi kisha akimbie.
Jamani, tunatakiwa kuwa makini sana tunapoingia kwenye uhusiano. Ni vigumu kumjua mtu mwenye mapenzi ya dhati kwako lakini unapokuwa na mtu ambaye hizi I love you, I miss you hazikauki, jaribu kumchunguza kwani huenda ni tapeli wa mapenzi.
Maneno siyo vitendo
Haya maneno ambayo hutolewa na watu wenye mapenzi ya dhati sasa hivi imekuwa ni tofauti. Unaweza kuitwa majina yote matamu, mara dear, my sweetheart, my love lakini kumbe anayekuambia anasema tu na wala hamaanishi kwamba yanatoka moyoni mwake.
Usiwe mbumbumbu na kudatishwa na maneno, kama kweli anakupenda vitendo vyake ndivyo vifanye kazi na siyo kulainishwa na ‘vijineno’ tena vya Kiingereza ambavyo yeyote anaweza kukuambia na wala asimaanishe hicho anachokisema.
Kwa leo, naomba niishie hapo nikiamini sasa utakuwa makini kuhakikisha hauingii kwenye penzi la Kichina......
No comments:
Post a Comment