UTATA kuhusu umri wa mtuhumiwa wa kesi ya
mauaji, mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ leo umeanza kutoa
matokeo, kwenye ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, huku kesi
yake ikipigwa tena kalenda hadi Mei 21, mwaka huu.
Lulu anayekabiliwa na kesi ya kumuua
mwigizaji mwenzake, Steven Charles Kanumba, kwa sasa anasema ana miaka 17, lakini
katika mahojiano kwenye kipindi cha TV cha Mikasi, kabla ya kifo cha The Great aliwahi
kusema ana umri wa miaka 18.
Wakili wa mwigizaji huyo aliyekulia kwenye
sanaa hiyo kuanzia akiwa kinda katika kundi la Kaole Sanaa la Magomeni pamoja
na marehemu Kanumba, Kenned Fungamtama leo aliwasilisha ombi katika Mahakama
hiyo, akiitaka iitupilie mbali kesi hiyo ili ikafunguliwe upya katika Mahakama
ya Watoto, akidai Lulu ana umri chini ya miaka 18.
Lakini Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Elizabeth Kaganda alipinga akisema suala hilo, inabidi kwanza lifanyiwe
uchunguzi na vyombo vya dola ili kugundua ukweli kuhusu umri wa Lulu(pichani kushoto).
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili Kaganda
alisema mbali na umri wa Lulu kuwa na utata, lakini hata jina lake halisi nalo ni
tatizo, pia kwani wakati wengi wanamfahamu kama Elizabeth Michael, lakini cheti
chake cha kuzaliwa kinasomeka Diana Elizabeth.
Katika ufafanuzi wake, Hakimu Mkazi, Augustina
Mmbando alisema analitupilia mbali ombi la upande wa utetezi, kwa sababu mtuhumiwa
anakabiliwa na kesi ya mauji na imefunguliwa chini ya Kifungu cha 196 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Alisema kwa mujibu wa kesi hiyo, Mahakama
yake haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo, zaidi ya Mahakama Kuu. Hakimu Mmbando
ameiahirisha kesi hiyo hadi Mei 21, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment