Social Icons

Tuesday, October 8, 2013

ALIYECHINJWA NA MUMEWE; MAPYA YAIBUKA

Stori: Makongoro Oging’
MAUAJI ya mwanamke aliyetambulika kwa jina la Zakia Omari,32, yanayodaiwa kusababishwa kwa kuchomwa kisu na Jumanne Ramadhani, eneo la Manzese Kwamfuga Mbwa jijini Dar es Salaam, mapya yameibuka, Uwazi linakupasha.
Marehemu Zakia Omari enzi za uhai wake.
Mara baada ya kifo cha Zakia kutokea  Septemba 28 mwaka huu katika nyumba ya mtuhumiwa, gazeti hili lilimtafuta  mama mkubwa wa marehemu aitwaye Rehema Matembele maarufu kwa jina la mama Chakida ambaye ameibua mapya.
Katika mahojiano na gazeti hili mama huyo alikua na haya ya kusema:
“Kifo cha mwanangu Zakia kimenishtua sana, ni mauaji ya kikatili na ya uonevu kwani katika kipindi chote walichoishi na huyo mwanaume alikuwa na mateso bila raha.
Mtuhumiwa Jumanne Ramadhani.
“Nakumbuka ya kwamba mama mzazi wa marehemu alifariki na kuniachia Zakia akiwa na umri wa miaka miwili, nilimlea hadi alipokua mkubwa na kumpata huyo mume aliyemuua.
‘Walikua wakiishi pamoja huko Mabibo na walibahatika kumpata mtoto mmoja aitwaye Ramadhani ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 13 na anasoma darasa la sita.
“Marehemu alikua akiishi na huyo mwanamume katika hali ya ugomvi mara kwa mara, hakuwa na raha hata kidogo.
 “Mwaka 2008 ugomvi wao ulipamba moto kwani marehemu alikuwa akifanya biashara lakini mtuhumiwa alikua akichukua fedha na kwenda kunywea pombe na akikataa kumpa alikuwa akipigwa.
“Waliendelea na ugomvi huo nakumbuka kuna siku alimchoma visu mara saba hadi mwanangu akalazwa Hospitali ya Sinza, ilibidi polisi wamkamate mwanaume huyo akafunguliwa kesi katika Mahakama ya Kinondoni.
“Mwanaume huyo aliomba sana na kumpigia magoti Zakia na akaamua kumsamehe na  kuachana naye na kurudi nyumbani.
“Nikawa naishi naye hapa Kimara akitafuta njia nyingine ya maisha na mwaka 2009, aliondoka hapa nyumbani akawa anafanya biashara ya Mama Lishe huko Manzese.
“Aliamua kuishi na wanaume mwingine aitwaye Haruna Said, ambaye amezaa naye watoto wawili, Aisha Haruna (7),  na Faulate,4.
“Taarifa nilizozipata siku hiyo ya tukio ni kwamba, Zakia akiwa kazini kwake alipigiwa simu na mtuhumiwa akimtaka aende nyumbani kwake Manzese Kwamfuga Mbwa akamchukulie mtoto wake vifaa vya shule.
“Niliambiwa hakutaka kwenda lakini wenzake walimsihi aende kwani hawezi kumfanya chochote.
“Saa moja jioni akafika kwa mtuhumiwa na hakuna anayejua kilichosababisha wagombane hadi akauawa.
“Tuliamua kuwachukua watoto wa marehemu na msiba tukahamishia hapa kwangu Kimara. Jumapili tulichukua mwili na kuusafirisha Mvomero, mkoani Morogoro kwa mazishi.
“Wakati huo mume wake aliyekua akiishi naye hadi kifo kinampata alikua amesafiri kikazi mkoani Tanga na alifika Jumatatu akakuta tumeshazika kwani mwili wa marehemu ulikuwa umeharibika sana,” alisema mama huyo huku akilengwalengwa na machozi.
Baadhi ya majirani eneo la tukio ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini kwa nyakati tofauti  walisema walisikia kelele za Zakia kuomba msaada kutoka katika chumba cha mtuhumiwa lakini hakuna aliyejitokeza kusaidia.
“Hatukuweza kujitokeza kwa sababu mtoto wa mwenye nyumba anayoishi mtuhumiwa alikua amekaa nje wakati huo na tulipomuuliza kuhusiana na kelele hizo alituambia kwa ni kawaida yao kugombana na wala hakuna kigeni,” alisema jirani mmoja.
Wengine walisema walimuona mtuhumiwa akitoka ndani mbio huku ameloa damu hali iliyowafanya wawe na hofu na kwenda hadi chumbani, walipofika walikuta mwili wa Zakia ukiwa katika dimbwi la damu hivyo kutoa taarifa polisi.
Mara baada ya polisi wa Kituo cha Urafiki kupata taarifa walifika  kuchukua maiti na kuipeleka Hospitali ya Muhimbili.
Habari zaidi zinasema marehemu aliacha simu yake nyumbani kwake na mara baada ya kufanya mauaji aliipiga simu hiyo ikapokelewa na mtoto wake aitwaye Rehema ambaye alimtaarifu kuwa mama yake amemuua hivyo waende kuchukua maiti, walienda na kukuta maiti imeshachukuliwa na polisi kupelekwa Hospitali ya Muhimbili.
 Baadhi ya majirani walidai kuwa mtuhumiwa alikuwa akibadilisha majina, mara alikuwa akijiita Jumanne Ramadhani lakini Kariakoo alikuwa akijulikana kwa jina la Kindombo na Manzese alijulikana kwa jina la Kichupi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camilius Wambura alisema: “Mtuhumiwa mpaka sasa hajatiwa mbaroni, tunawaomba wananchi wakimuona popote watoe taarifa kituo chochote cha polisi ili afikishwe mahakamani kwa unyama alioufanya.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment

 

for more information call us

+255718953088
-------or-------
+255784953088
*email*
innocentfabian@gmail.com
THANKS

quote of the day

"Don't criticize me simply because I am different. Understand me, and you will most likely appreciate my difference and criticize your variance."