HAPA
ndiyo sehemu pekee ya kupanua mawazo na kukuza ubongo wako juu ya mambo
yanayohusu uhusiano na mapenzi. Kama ni mara yako ya kwanza kuanza
kupitia ukurasa huu, umekutana na kona muhimu sana. Huna cha kupoteza.
Utajengeka kila siku.
Rafiki
zangu, leo nimekuja na mada mpya baada ya kuhitimisha ile ya wiki
iliyopita. Nina imani kuna mengi mliyojifunza. Mada ya leo inatokana na
maswali mengi ya aina moja niliyoyapata kwa muda mrefu kutoka kwa
wasomaji mbalimbali.
Hebu
msikie huyu: “Pole na kazi kaka Shaluwa, kuna kaka nawasiliana naye.
Kiukweli tumezoeana sana, juzi hapa amesema eti ananipenda na anataka
kunioa. Mimi nipo Mbeya, yeye anaishi Dar es Salaam.
“Hatujawahi
kuonana, zaidi ya kuzungumza kwa njia ya simu tu. Nilifahamiana naye
baada ya kukosea namba, ndipo tukakubaliana kuwa marafiki. Tafadhali
naomba msaada wako maana ninachanganyikiwa kabisa. Ni kweli
ananipenda?”.
Kilio
kama hicho nilikipata pia kutoka kwa msomaji mmoja ambaye naye
sitachapa jina lake gazetini. Huyu alisema: “Nimekutana na rafiki kwenye
Facebook, tunawasiliana mara kwa mara, ninahisi kumpenda huyo msichana.
Naye ana kila dalili za kunipenda, tatizo sijaanza tu kumweleza. Hivi,
inawezekana kweli tukapendana kabla ya kuonana?”
Bila
shaka kuna picha umeipata kupitia maswali ya wasomaji hao wawili.
Niliwaahidi kuandika mada gazetini ambapo ndipo wangepata majibu yao.
Je, wewe upo kwenye kundi gani?
Umewahi
kukutana na jambo hilo? Unadhani unaweza kumpenda mtu kabla ya kukutana
naye? Sauti pekee inaweza kumfanya mtu ampende mwenzake kwa dhati na
mapenzi yao yakadumu? Twende tukajifunze.
INAWEZEKANA?
Hili
ni jambo la kwanza linalotakiwa kupatiwa majibu kabla ya kuendelea na
mada hii. Huu ni mtazamo hasi. Jibu kwa kifupi tu ni haiwezekani.
Utawezaje kumpenda mtu ambaye hujamuona?
Misingi
ya kumpenda mwingine ikoje? Kanuni zipo wazi; KUPENDA ndiyo jambo la
kwanza, ambapo ukweli ni kwamba huanza na kutamani, sasa itawezekanaje
kumtamani mtu ambaye hujawahi kukutana naye?
Baada
ya kupenda, kuna mambo mengine ya msingi ambayo ni muhimu kuzingatiwa
ili kujihakikishia kwamba uliyempata ni mwenzi sahihi. Kuna suala la
kuchunguzana tabia n.k, yote haya yatawezekana vipi kufanyika kabla ya
kukutana?
Najua
ni wengi wamekumbana na hili ninalolizungumzia hapa, unashindwa cha
kufanya na kubaki gizani. Leo utarudi kwenye mwanga! Unajua chanzo cha
yote hayo ni nini? Twende kwenye kipengele kinachofuata.
HUANZA HIVI...
Chanzo
kikuu cha udanganyifu huu wa mapenzi huwa ni vyombo vya mawasiliano.
Mfano mtu amepiga simu amekosea namba...mara anaanza ‘uko wapi? Haina
neno, tunaweza kuwa marafiki?’
Mazoea
yakizidi, kila mmoja huanza kumwuliza mwenzake vitu anavyopendelea na
mambo mengine. Baadaye wanatongozana! Huelezana mambo mengi sana na
ahadi nyingi wakiamini kwamba wanapendana kwa dhati!
MAPENZI YA HISIA
Kimsingi
sababu ya haya yote ni hisia tu. Njia ya mawasiliano inaweza kukoleza
au kuimarisha uhusiano ambao tayari upo. Mfano kama unaishi Moshi na
mpenzi wako yupo Mwanza, mnaweza kuboresha uhusiano wenu kwa kuwasiliana
kwa njia ya simu, waraka pepe na mitandao ya kijamii.
Kinachotokea
kwa marafiki wapya ambao wanahisi tayari ni wapenzi na wanapendana ni
zile hisia za ndani zinazowaingia wakati wa mawasiliano yao. Pengine
walianza kuzungumzia mambo ya mapenzi na kujikuta wakitamani kuwa
karibu.
Jambo
kubwa zaidi ni kwamba mhusika hutawaliwa zaidi na hisia, maana kwa
sababu hawafahamiani, watakuwa wanauliza; ‘Wewe ukoje? Mrefu, mfupi,
mwembamba, mnene au?’ halafu mwenzake atamjibu, ‘mrefu kiasi, si mnene
sana, kifupi nina umbo namba nane...navutia na ni maji ya kunde’.
Kifupi
mtu anaweza kujielezea vyovyote atakavyo, hivyo kumfanya mwenzake
amtengeneze ajuavyo kichwani mwake na kujihakikishia kwamba anampenda
kwa dhati mwenzake kumbe anajidanganya!
TABIA BANDIA
Mbaya
zaidi ni kwamba, wakati wapenzi hawa wanaojidanganya wakiendelea
kuwasiliana si rahisi kujuana vizuri kitabia kwa sababu wengi huonesha
tabia bandia. Mambo yao ya ndani wanayaficha kwa nguvu na kuonesha mema
tu.
Hapo ndipo mwanzo wa penzi feki kwa kudanganyika na tabia za kutengeneza.
HULKA MBAYA
Kuna
wengine ni tabia zao za asili. Amezoea kupata wapenzi kwa kupitia
kwenye simu na mitandao ya kijamii. Usishangae kuna wengine wanapiga
namba hata wasizozijua, akikutana na mtu wa jinsia tofauti na yake,
anaanza mambo yake. Akimaliza haja zake anakuacha!
ACHA KUJIDANGANYA
Ni
vizuri sasa ukatoka kwenye ulimwengu wa giza na kurudi kwenye ulimwengu
unaonekana. Kwa hakika ni vigumu sana kumpenda mtu ambaye hujamuona,
labda kama unataka kucheza na muda wako.
Wako
anakuja, vuta subira ukifanya mambo yako kwa usahihi. Usijidanganye na
matapeli wa mapenzi. Wapo ambao wanafanikiwa kuingia kwenye mapenzi
lakini mwisho wao hauwi wenye mafanikio.
Penzi
la dhati hubebwa na vitu vingi sana, ukiachana na UPENDO kuna suala la
tabia na mengine mengi ambayo huwezi kuyajua kwa njia ya kuwasiliana
pekee. Utajihakikisha umempenda kwa kumtengeneza kichwani mwako, mwisho
wa siku unakutana na mtu ambaye yupo tofauti na mawazo yako, itakuwaje
hapo?
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya
Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love
na Who is your Valentine? vilivyopo mitaani.
KWA HABARI ZAIDI ZA MAHUSIANO NA NYINGINE INGIA:
No comments:
Post a Comment