MWANAFUNZI wa mwaka wa pili katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kilichopo Njiro jijini hapa, Henry Koga, ameuawa kikatili na hivi ndivyo alivyouawa.
Enzi za uhai wa mwanafunzi huyo
Kwa mujibu wa wanachuo wenzake ambao hawakutaka majina yao kuandikwa
gazetini, Koga aliuawa kinyama kwa kuchomwa kisu shingoni na kundi la
watu wasiofahamika wakati akitoka kujisomea nje ya chuo usiku wa kuamkia
Jumatano iliyopita.Imeelezwa kuwa tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo lilitokea saa 4 usiku ambapo marehemu huyo akiwa na wenzake walivamiwa na kundi la wahuni wapatao wanne katika eneo la CDA, jirani na chuo hicho na Koga kuchomwa kisu shingoni na kifuani.
Wanachuo wenzake walisema marehemu hakuwa anatoka kwenye starehe kama watu wengine wanavyodai bali alikuwa na wenzake wakitoka kujisomea nje kidogo ya chuo hicho kwa ajili ya kujiandaa na mitihani na walipofika eneo hilo, wakavamiwa na watu wasiojulikana.
Baada ya tukio hilo, baadhi ya wanafunzi walijikusanya asubuhi yake na kuanza kuandamana kushinikiza uongozi wa chuo hicho kutoa tamko juu ya vitendo vya uhalifu vinavyojirudia mara kwa mara chuoni hapo.
Kufuatia tukio hilo, wanachuo hao walifanya vurugu kubwa na kumlazimisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo kwenda chuoni hapo, alipofika kulitokea hali ya kutoelewana ambapo walimzomea na kumpiga mawe, hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na kuwafyatulia mabomu ya machozi.
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema naye alijitahidi kuwatuliza bila mafanikio huku ikidaiwa yeye ndiyo chanzo cha vurugu hivyo kutakiwa kukamatwa. Mkuu wa mkoa alilazimika kuondoka eneo kuokoa maisha yake.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Ibrahimu Kilongo akizungumzia tukio hilo, alisema wanachuo 10 wanashikiliwa na polisi kutokana na vurugu hizo na kwamba uchunguzi unaendelea.
No comments:
Post a Comment