Social Icons

Thursday, April 25, 2013

Wanaume wanavyoibiwa kwa ‘I love U, I miss U baby!’

Ndugu zangu, wiki hii nataka kuzungumzia suala moja ambalo nahisi wanaume wengi hawalifahamu. Kwa kifupi ulimwengu wa mapenzi wa sasa umetawaliwa na usanii wa hali ya juu.
Wanawake wengi wameyageuza mapenzi kama kitega uchumi. Wapo ambao hawataki kusikia suala la kuwa na wapenzi wala kuolewa wakiwa na dhamira ya kutaka kuwa na uhuru wa kuwabadili wanaume kadiri wanavyotaka.
Unaweza kukutana na msichana mzuri sana, ukampenda na kudhani anaweza kuwa mkeo. Yeye akishabaini umemzimikia, anakuwekea mapozi ya kimtindo kwa muda kisha anakukubalia.
Kwa kuwa na wewe umeoza kwake, utakuwa tayari kumfanyia chochote ili uweze kumshikilia. Akilini mwako unajipa matumaini kuwa uko peke yako na huyo atakuwa mkeo siku zijazo kumbe mwenzako ana lengo la kukuchuna tu.
Atatumia maneno matamu kukulainisha lakini mizinga itakuwa sehemu ya maisha yake. Kwa kuwa na wewe unampenda na hauko tayari kumkosa, utakuwa ukimpa pesa na huduma nyingine.
Unajua kitakachotokea? Huenda hujui lakini wengi wanafanya hivi; anakupiga mizinga sana hadi inafikia hatua unamchukia na kuhisi hakufai.
Kuhisi kwako hakufai ndiyo furaha kwake kwani na yeye hakuweka akilini mwake kuwa anataka kuolewa na wewe. Matokeoa yake unabaki ukiumia kumkosa na pia itakuuma zaidi kwa kuwa ametumia pesa zako nyingi bila kufanikisha kile ulichodhamiria.
Hivyo ndivyo ilivyo sasa na kwa mfano kuna hii mitandao ya kijamii kama vile Facebook. Huku wanaume wengi wanalizwa na hawa mabinti wajanja wa mjini.
Msichana anaweza kukuomba urafiki ukamkubalia, baada ya muda anajitongozesha kwako kwa kudai amekuzimikia. Kama na wewe utakuwa limbukeni na ukadata na mtu ambaye wala humjui lakini maneno yake yakakuvutia, tarajia kulizwa.
Nasema hivyo kwa kuwa, ni lazima ataonesha kukupenda sana na atakuwa akikuandikia maneno matamu kama vile I love you, I miss you na mengineyo ya aina hiyo na ukishakolea si ajabu akaanza kukuambia anataka kuonana na wewe ila kwa kuwa yuko mbali anataka umtumie nauli.
Lakini hata kabla ya kukuambia umtumie nauli, anaweza kuwa ameshakuomba pesa nyingi, vocha za kutosha na wewe ukawa unamtumia ili kulilinda penzi lenu.
Sasa mwisho wa mawasiliano yenu utakuwa pale ambapo atakuomba umtumie nauli ili aje muonane, ukishamtumia tu anaingia mitini na huwezi kuamini msichana huyo anaweza kuwa na wanaume wengi anaowafanyia hivyo.
Wengine hawatumii mtandao wa Facebook bali hutumia simu zao kuwaingiza mjini wanaume. Kwa kifupi huo ni mchezo ambao upo na wanaume wengi wameshalizwa.
Kikubwa ni watu kuwa makini na hawa wasichana warembo wanaojirahisi kwa wanaume. I love you, I miss you ni maneno tu ambayo anayeyatamka anaweza akawa hamaanishi hivyo bali anataka kukupumbaza tu na ukiingia kwenye laini akuchune weee mpaka mwenyewe uachie ngazi kisha yeye anahamia kwa mwingine.

Ni hayo tu kwa leo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment

 

for more information call us

+255718953088
-------or-------
+255784953088
*email*
innocentfabian@gmail.com
THANKS

quote of the day

"Don't criticize me simply because I am different. Understand me, and you will most likely appreciate my difference and criticize your variance."