Social Icons

Wednesday, May 8, 2013

JIDE ANA HOJA, RUGE NAYE ANA HOJA PIA!

KWENU,
Wadau wa burudani Bongo. Salaam sana. Nalazimika kusema kitu tena kuhusu suala la mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na Radio Clouds FM ya jijini Dar es Salaam.
Mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’.
Najua wengi mnafahamu juu ya mgogoro ulioanza chinichini kati ya Jide na redio hiyo huku akiwataja moja kwa moja viongozi wa juu wa redio hiyo, Joseph Kusaga aliye mkurugenzi mtendaji na Ruge Mutahaba ambaye ni mkurugenzi wa vipindi.
Kwa jumla, Jide alianza kwa kugusagusa bila kueleza hoja moja kwa moja. Nakumbuka wiki iliyopita nilimwandikia barua nikamshauri aachane na vita ya chinichini kama ni kweli ana ushahidi anaonewa na wasanii wengine wanaomfuata waweze kunufaika na vita yake.
Jide alifikia mahali akaanza kuwadisi hadi waandishi ambao ndiyo waliosaidia kufikisha hili sakata lilipofikia. Nilimweleza wazi, kwamba alifanya makosa.
Niliona kweli ana hoja lakini njia aliyoitumia haikuwa sahihi. Alipaswa kujipanga na kukutana na wasanii wenzake (kama ni kweli alikuwa akipigania haki za muziki wa Tanzania kama alivyosema kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii) ili wajipange kwa mapambano.
Meneja wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
Baadaye akaandika kitu kingine kilichoshangaza zaidi, alizungumzia kuporwa wanamuziki wake na kuingiliwa kwenye biashara, kisha akafunga kwa kudai kwamba, hao ‘wabaya’ wake wasimzike ikitokea amekufa kabla yao.
Yale yalikuwa maneno mazito sana, ndiyo maana mwisho wa siku nilishauri ni vyema hizi pande mbili zikakutana na kujadiliana. Nilihisi kama kuna hoja binafsi zaidi ambazo Jide alishindwa kusema ndiyo maana waandishi walimchokonoa ili azungumze.
Juzi, Jumatatu Mei 6, 2013, Ruge aliamua kuvunja ukimya kupitia Kipindi cha Power Breakfast ya Radio Clouds FM na kumjibu Jide. Nilimsikiliza kwa makini sana. Alizungumza kwa umakini mkubwa na kutumia busara iliyotosheleza.
Kwamba, vita ya kwenye mitandao ya kijamii haina maana na haikuwa na maana. Kwamba, Jide anafahamu alipokosea na njia za utatuzi pia anazijua.
Alifafanua kwamba mgogoro ulioanzishwa na Jide ni hitilafu za kibiashara ambazo ni binafsi na zinazoweza kumalizika kwa njia ya mazungumzo kwenye meza moja, si kwa kuchafuana majina mitandaoni.
Ni kweli, suala la wimbo kutopigwa kwenye kituo fulani si suala la kitaifa kama alivyosema Ruge mwenyewe. Ni binafsi linalohitaji busara kutatua.
Bado njia iliyo bora ya kumaliza mgogoro huu kama nilivyosema mwanzo ni kukutana kwenye meza ya mazungumzo. Hata kama kuna makosa mengine ambayo mmeshindwa kuyaweka wazi lakini naamini kwa safari mliyoanza pamoja karibu miaka 10 iliyopita, inatosha kuwafanya muwe na busara ya kukubali kukutana na kuzungumza.
Nashukuru Ruge ameweka wazi kwamba, Jide anayo nafasi ya kukutana nao na kuzungumza ili kuona wazi kama kuna tatizo na kurekebisha. Ni kweli wote mna hoja za msingi ila sasa ili muende sawa, kutaneni kwenye meza ya mazungumzo.
Ruge yupo tayari, Kusaga yupo tayari, Clouds wapo tayari. Kazi kwako Jide a.k.a Komando.
Yuleyule,
Mkweli daima,
Joseph Shaluwa  
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment

 

for more information call us

+255718953088
-------or-------
+255784953088
*email*
innocentfabian@gmail.com
THANKS

quote of the day

"Don't criticize me simply because I am different. Understand me, and you will most likely appreciate my difference and criticize your variance."