Social Icons

Wednesday, May 8, 2013

SHAMBULIO LA BOMU KANISANI... HAWA WANAHUSIKA?

Na Mwandishi Wetu, Arusha
TUKIO la bomu lililotupwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit, Arusha, linazidi kuumiza vichwa vya Watanzania, kiulizo tata kikipamba swali la ni yupi mhusika kati ya makundi matatu yanayotajwa.
Mmoja wa majeruhi wa mlipuko wa bomu lililotupwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit, Arusha.
Wapo maadui watatu ambao wapo kwenye fikra za Watanzania kwamba mmojawapo ndiye sababu ya mlipuko huo ambao mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni, ulikuwa umesababisha vifo vya watu wawili pamoja na majeruhi 42.
Hali halisi iliyopo nchi kwa sasa, imesababisha makundi matatu kuhusishwa, mawili kutoka nje ya Tanzania lakini moja ni la ndani.
KWA NINI MAKUNDI MATATU?
Msimamo wa Tanzania dhidi ya amani ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imesababisha kugeuka adui wa waasi wa nchi hiyo ambao ni Kundi la M23.
Magaidi wa Kundi la Al Shabaab ni watajwa wengine, kwani baada ya kufanya ugaidi kwenye nchi za Somalia na Kenya, walisharipotiwa kujipenyeza nchini, hivyo inadhaniwa pengine wameanza utekelezaji wa uharamia wao.
Kundi la tatu ambalo linashukiwa hata na serikali kutokana na nukuu za baadhi ya viongozi, ni watu wasiojulikana ambao wanawekeza nguvu zao katika kueneza chuki za kidini kwa lengo la kuwagawa Watanzania.
Baadhi ya wanajeshi wa kundi la M23.
KUNDI LA M23
Bomu hilo la mkono, lilirushwa kanisani Mei 5, mwaka huu (Jumapili iliyopita), saa 4:30 asubuhi. Siku moja kabla, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alitoa tamko la serikali kuwa Tanzania lazima ipeleke majeshi DRC kupigania amani na haitishwi na vitisho vya M23.
Kauli ya Membe, ilifuatia waraka wa M23 ambao waliutuma nchini, wakieleza kuwa ni ujumbe kutoka kwa Mungu, wakiionya Tanzania kutopeleka majeshi DRC, vinginevyo itakiona cha moto.
Baada ya kauli hiyo ya Membe, M23 walihamishia mashambulizi yao kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, wakiitishia Tanzania.
Baadhi ya ‘twiti’ za M23 Jumamosi iliyopita baada ya tamko la Membe, mojawapo inasema: “Membe usiwadanganye watu, mnakuja DRC kuweka petroli kwenye moto, hamji kutafuta amani.”
Twiti nyingine inasomeka: “Hatutishwi na scout (askari chipukizi), Tanzania leteni majeshi yenu halafu mtaona.”
Hatari kubwa zaidi ni kwamba M23, walitishia kuingia nchini na kufanya mashambulizi, wakitamba wana uwezo mkubwa sana wa kufanya hivyo.
Siku hiyohiyo (Jumamosi), Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ‘alitwiti’, akionya kwamba M23 walikuwa ‘wanatwiti’ wakiwa Dar es Salaam, hivyo ni dhahiri kuwa kundi hilo lilikuwa limeshaingia nchini.
Hivyo, kitendo cha bomu kulipuka siku moja baada ya malumbano, kimetoa ishara kuwa pengine M23, walifanya shambulio la awali kama jaribio kuelekea katika kutimiza azma yao.
Baadhi ya wanajeshi wa kundi la Al-Shabaab.
AL-SHABAAB
Ilisharipotiwa kuwa Kundi la Al Shabaab limeshaingia nchini, vilevile yapo madai kuwa magaidi hao wapo wanakusanya nguvu kabla ya kuanza utekelezaji wa matukio yao ya kigaidi nchini.
Kuenea kwa madai hayo na wasiwasi uliopo ndani ya Watanzania kwa sasa, imekuwa sababu ya Al Shabaab kuwa moja ya makundi ambayo yanatajwa kuhusika na shambulio la bomu Arusha.
KUNDI LA TATU
Machafuko ya kiimani nchini, yamesababisha kuibuka kwa tuhuma kwamba lipo kundi hatari ambalo lenyewe kazi yake ni kupandikiza chuki za kidini miongoni mwa Waislamu na Wakristo ili waumini wake wapigane na damu imwagike nchini.
Kumekuwa na uchochezi wa hali ya juu, Wakristo na Waislamu wakipandikiziwa mbegu ya kuchukiana. Kundi linalohusika na uchochezi huo, linahisiwa kuwa lililipua bomu hilo kanisani ili Wakristo waamini shambulizi limefanywa na Waislamu.
Kabla ya tukio hilo la kanisani, wiki zilizopita, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Arusha, Sheikh Abdulkarim Jonjo, alishambuliwa na bomu akiwa nyumbani kwake na kujeruhiwa vibaya.
“Binafsi naamini kuna wasaliti ndani ya nchi yetu ambao wameamua kuivuruga amani yetu. Sheikh Abdulkarim alipojeruhiwa na bomu, wachochezi walitaka Waislamu waelekeze chuki zao kwa Wakristo lakini haikuwa hivyo.
“Inawezekana kabisa, watu waliomrushia bomu Sheikh Abdulkarim ndiyo haohao waliolishambulia kanisa. Inabidi tuwe makini sana. Tukidanganyika, tunaweza kupigana sisi kwa sisi. Hakuna Muislamu Mtanzania anayeweza kumdhuru Mkristo, vilevile Mkristo hawezi kumdhuru Muislamu kutokana na asili yetu na tunavyojijua,” alisema Elibariki Shayo wa Kijenge Chini, Arusha.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
KAULI KALI YA WAZIRI NCHIMBI
Kuonesha kwamba serikali inalibeba kundi la tatu kama mtuhumiwa nambari moja, Jumatatu iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kuwa watu wanaoeneza chuki za kidini hawatavumiliwa, watachukuliwa hatua kali sana.
“Tunaendelea na uchunguzi wetu lakini kuanzia sasa, serikali haitawavumilia watu wanaoeneza chuki za kidini, tutawachukulia hatua kali ili iwe fundisho,” alisema Nchimbi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete.
JK ASITISHA SAFARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, alikuwa kwenye ndege safarini kwenda Kuwait, wakati shambulio hilo la bomu lilipofanyika lakini alipofika na kujulishwa kilichotokea, alisitisha ziara yake na kurudi nchini.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na viongozi mbalimbali nchini kwa ajili ya kupata picha halisi ya tukio.
“Sasa hivi (Jumatatu mchana), yupo njiani, atafika Dar es Salaam halafu kesho asubuhi atakwenda Arusha,” alisema Rweyemamu.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
LEMA AZIDI KUKOSOLEWA
Kauli ya utata ambayo Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, aliitoa akiilaumu serikali kukumbatia udini kwamba ndiyo chanzo cha shambulio hilo, imezidi kukosolewa.
Caroline Moroli, 34, aliyekuwa Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi wakati mlipuko unatokea, alisema: “Nilikuwepo hapa namshukuru Mungu nimepona, nilimsikia Lema, kwa kweli alinisikitisha sana. Ile kauli ni mbaya sana.
“Hakuna udini hapa, hili tukio ni la kigaidi. Viongozi wetu wasipandikize mbegu za chuki ya kidini, ni jambo baya sana. Nashauri serikali ifanye uchunguzi, hawa magaidi wakamatwe. Mimi ni Mkristo na sikubaliani na haya maneno kuwa Waislamu wanaweza kuhusika.”
Caroline, anaungana na wakazi wengine wa Arusha ambao walinukuliwa na gazeti mama la hili la Uwazi ambao walieleza jinsi wanavyompenda Lema na kumheshimu lakini wanashangazwa na kauli yake tata, hivyo wakamtaka aache siasa kwenye mambo nyeti kama hayo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment

 

for more information call us

+255718953088
-------or-------
+255784953088
*email*
innocentfabian@gmail.com
THANKS

quote of the day

"Don't criticize me simply because I am different. Understand me, and you will most likely appreciate my difference and criticize your variance."